Dk. JOHN POMBE MAGUFULI

Vance Ngimba
3 min readMar 26, 2021

--

Rais John Pombe Joseph Magufuli

Mwaka 2015 nikiwa kijana mdogo na mfuasi wa chama cha CHADEMA (Chama cha Demokrasia na Maendeleo) nilikua njia panda kuchagua kati ya Edward Lowassa na John Pombe Magufuli kuwa rais ajae wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa awamu ya 5.

Edward Lowassa. Alikua ni mtu alikua na wafuasi wengi sana kipindi hicho pengine kuliko kipindi chochote cha uchaguzi kutokea hapo nyuma. Alikua kada mtiifu wa CCM (Chama Cha Mapinduzi) kwa muda mrefu sana lakini aligubikwa na kashfa za rushwa, ambazo hazikuwahi kutibitishwa na mahakama. Alikua mchapa kazi. Mwenye mvuto. Tajiri. Alikua ni kiongozi aliejiandaa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa muida mrefu ambae kila mtu aliamini kwamba ndie kiongozi atakaefuata baada ya Rais Dk. Jakaya M. Kikwete. Upinzani (Vyama vya kisisasa vinavyotengeneza umoja wa upinzani Tanzania) ulizunguka kutuaminisha kwamba alikua ni mwizi na fisadi mkubwa wa mali za Umma nchini Tanzania. Na mimi nikiwa kama mfuasi kindakindaki wa CHADEMA niliamini hivyo. ‘Lowassa na CCM ni wezi wanaoliletea Taifa umasikini mkubwa’.

Baada ya mchakato wa kutafuta mpeperusha bendera wa CCM kuisha na Lowassa ‘kuchinjwa’ alihamia CHADEMA na kupitishwa kuwa mgombea wa Urais, nafasi ambayo mwanzo alipewa Dk. Wilbroad Slaa ambae ndio alikua mgombea wa nafasi hio kwa miaka mitano iliyopita. Dk. Slaa aliombwa kutoka na kumpisha mgombea aliekuja Lowassa kuwa mgombea rasmi wa UKAWA. Huyu ndio Lowassa ambae viongozi wetu wa upinzani kwa miaka takriban 10 walituaminisha kuwa na mwizi na fisadi mkubwa siefaa kushika nyadhifa yoyote kwenye nchi hii. Dk. Slaa nae akaamua kukikacha Chama cha Demokrasia Makini ni kuondoka zake.

Upande wa CCM chama Tawala walimsimamisha Dk. John Pombe Joseph Magufuli, hapo akiwa Waziri wa Ujenzi wa Serikali inayomaliza muda wake chini ya Dk. Jakaya Mrisho Kikwete. Rekodi ya Magufuli ilikua safi na ya kuvutia. Mtekelezaji. Asie na woga. Mtiifu. Mwaminifu. Asiekuwa na maneno mengi. Mchapa kazi. Jembe. Mpambanaji. Muelewa. Mcha Mungu. alipitishwa baada ya kasheshe na mbilingembilinge nyingi na porojo zisizo na maana za Chama cha Mapinduzi. Dk. J. P. J. Magufuli akateuliwa kupeperusha bendera ya CCM kwa mwaka 2015.

Mimi kama mpiga kura nikiwa na miaka 24 kipindi hicho mpaka naingia kwenye chumba cha kupigia kura nilikua sijaamua nani nimpe kura yangu kwa kiti cha Rais. Je, nimpe Lowassa anaegombea kupitia tiketi ya chama changu cha CHADEMA ambae tulikua tukimuita ‘Fisadi papa’ au JPM ambae ni mtu mwadilifu akipepperusha bendera ya CCM ambacho kilikua ni chama cha hovyo?

Wabunge na madiwani nilichagua wa CHADEMA. Rais baada ya kumuomba Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema nilimchagua Dk. John Pombe Joseph Magufuli. Kura ambayo nitaienzi na kuiheshimu na kujivunia maishani mwangu mwangu mpaka siku ile nitarudi kaburini. Mheshimiwa John P. J. Magufuli alinipa raha, heshima, ndoto, ari, nguvu na kupanua fikra zangu kwa kiwango kikubwa sana.

Nilimuamini sana katika utendaji wake kwa miaka yote ya Urais wake, nilimpenda, nilimheshimu, na ndio Rais pekee nilimuombea kwenye sala zangu na nitaendelea kumuombea. Nilimpigia tena kura mwaka 2020 ambapo alitawala kwa miezi michache tu mpaka umauti ulipomfika tarehe 17 Machi 2021. Jiwe, Jembe, Chuma…hakuna atakaetokea mwenye uwezo japo nusu yako. Uondokaji wako umetuuma sana baba. Nilimuuliza Mungu wangu wa mbinguni na muumbaji wangu kwanini ameyaruhusu haya ila jina lake kuu lihimidiwe na mapenzi yake makuu yatimizwe. Sisi ni wake nalbda John Magufuli muda wake wa kuwa kiongozi wa Malaika umetimia.

Dk. John Pombe Joseph Magufuli nenda baba mbele yako nyuma yetu sisi tutakuombea mpaka pale wasaa wetu wa kuitwa na Mungu Baba utakapowadia.

Dk. Magufuli umetenda mengi mno ambayo nitaandika siku nyingine ila la msingi umetujengea kujiamini, heshima, utu, uzalendo na misuli ya ufikiri miongoni mwetu. Nakulilia kimya kimya Rais wangu mpenzi, nitakuenzi siku zote za maisha yangu role model wangu. Na kama hatukushikana mikono kwenye maisha haya basi tutashikana kwenye maisha yajayo. Siamini kama leo Tarehe 26 Machi 2021 ndio mwisho wa kukuona duniani. Mungu akinibariki nitafika ulipolazwa kushuhudia labda ndio nitakubaliana na hali. Tutakuombea Mheshimiwa Rais. Tunakuombea JPM. Pumzika kwa amani.

Nitakuenzi daima. Na vizazi vyangu vitakujua na kukuheshimu.

Ulale mahala pema peponi Dk. John Pombe Joseph Magufuli wasalimie Sokoine, Mwalimu Nyerere na Benjamini Mkapa. Wewe ni mwamba imara uliejengwa kwenye fikra za watu na ndani ya mioyo yetu.

Mungu wetu mwenye rehema akusamehe dhambi zako na ukasherehekee na watakatifu na malaika wa mbinguni.

Kwa hakika umepigana vita vilivyo vizuri, mwendo umeumaliza, imani umeilinda. Amina

--

--

No responses yet